Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Friday, September 2, 2011

Mbozi yapewa fedha zaidi ya halmashauri zote Mbeya

Na Joachim Nyambo,Mbozi.

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbozi imetengewa shilingi 39,967,258,000
katika mwakaa wa fedha wa 2011/2012 ambapo kati ya fedha hizo shilingi
31,652,999,980 ni kwaajili ya mishahara na matumizi mengineyo na
shilingi 8,314,259,000 ni kwaajili ya miradi ya maendeleo ya wananchi.

Kiasi hicho cha fedha kimetajwa kuwa kikubwa ikilinganishwa na kiasi
kilichotengwa kwa halmashauri nyingine zote za mkoa wa Mbeya.

Licha ya halmashauri hiyo kutengewa kiasi hicho cha fedha kutokana na
kupata hati safi katika mwaka wa fedha 209/2010 kwa mujibu wa taarifa
ya mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali CAG halmashauri hiyo
imeshindwa kujibu hoja 18 kati ya 42 za mwaka huo wa fedha hivyo
kuifanya hati yao safi kuwa ya mashaka.

Baadhi ya hoja ambazo hazikujibiwa ni pamoja na kutotumika kwa wakati
muafaka kwa shilingi milioni 199.2 fedha za miradi ya afya
MMAM,Kutotumika kwa soko la mazao lililopo katika mji mdogo wa
Tunduma,kutokamilika kwa miradi ya Capital Development Grant (CDG)
pamoja na miradi saba ya kilimo ya ASDP.

Akizungumza juzi katika kikao cha maalumu cha baraza la madiwani cha
kujadili taarifa ya CAG kwa kipindi hicho,mkuu wa mkoa wa Mbeya John
Mwakipesile alisema kutokamilika kwa miradi hiyo kwa wakati
kuliwakosesha wananchi kupata unafuu wa maisha kama ilivyotaraajiwa
hivyo maendeleo yao kukwama.

Mwakipesile pia alisema kutotumika kwa fedha katika kipindi
kilichopangwa ni makosa kimahesabu kwakuwa thamani ya fedha
inabadilika hivyo kuchelewa kutumika kunaweza kusababisha mradi husika
kutokamilika.

“Thamani ya fedha ya juzi si sawa na ya leo.Mnaposhindwa kutumia fedha
kwa wakati uliopangwa ni makosa kihasibu kwakuwa mnaweza kusababisha
mradi kukwama.Na mwaka huu mmepewa fedha nyingi kwaajili ya miradi ya
maendeleo,mkikaa mkao wa kimaendeleo ni fedha nyingi lakini mkikaa
mkao wa kuzitafuna kifisadifisadi wananchi hawataona maendeleo yoyote”
alisema.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment