Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Tuesday, December 4, 2012

VIJANA WAJITOSA KUFANYA USAFI MBALIZI

VIJANA wa Mji mdogo wa Mbalizi uliopo katika wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani hapa, wanatarajia kufanya usafi katika mji huo kwa lengo la kuufanya mji huo kuwa safi na kuonesha uzalendo wao kwa nchi.

Taarifa iliyosainiwa na mratibu wa Vijana hao Gordon Kalulunga na kutumwa kwa vyombo vya habari jana, imesema kuwa dhumuni la usafi huo ni kuonesha uzalendo wao kwa taifa na kuwafanya vijana kutambua kuwa si kila jambo wanapaswa kulipwa.

‘’Kwa  Uzalendo wetu kwa nchi yetu bila kujali itikadi zetu za siasa wala dini na rangi zetu tumeamua kwa pamoja kufanya usafi wa mazingira katika mji wetu kwa kujitolea wenyewe bila ufadhili wa mtu yeyote na tutafanya hivyo kila mara’’ alisema Kalulunga.

Alisema kwa kuanzia watakutana kesho Jumatano eneo la Stendi ya Mbalizi huku kila mmoja akiwa na kifaa chake cha kufanyia usafi zikiwemo sululu, mifagio na koleo kisha watazibua mitalo na kufagia.

Kalulunga aliongeza kuwa baada ya hapo watafanya tathimini na kujiwekea malengo ya kufanya usafi kama huo katika eneo linguine na kwamba mwitikiowa vijana wa eneo hilo ni mkubwa na kwamba pia baadhi ya vijana kutoka Jiji la Mbeya wameomba na kuthibitisha kuwa watahusika kuonesha uzalendo wao kwa kujumuika na wenzao.

‘’Tukio hilo ni kubwa, tunaamini kwa kushirikiana na Serikali na wananchi wengine wazalendo tutashinda na kuiletea maendeleo jamii yetu na kutokomeza magonjwa yanayotokana na uchafu wa Mazingira na kwa kufanya hivyo tunaamini kila mmoja atatimiza wajibu wake kwa Taifa letu la Tanzania badala ya kutegemea kufanyiwa kila kitu na Serikali’’ alisema Kalulunga.

Aliongeza kuwa kabla ya zoezi hilo wametoa taarifa kwa viogozi wa Serikali akiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkuu wa wilaya, Afisa Mtendaji wa kata ya Utengule Usongwe, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbalizi na Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho.

Aliwaomba vijana wote ambao wapo tayari kushirikiana na wenzao bila malipo wajitokeze kufanya usafi huo na kujadiliana zaidi na wenzao kwa lengo moja la kuiletea maendeleo jamii na kuiepusha na magonjwa ya mlipuko kwa kufanya usafi katika maeneo watakayokubaliana na kuyabainisha.

No comments:

Post a Comment