Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Saturday, December 29, 2012

POLISI YAONYA VIONGOZI WA DINI,WANASIASA

VIONGOZI wa madhehebu ya kidini na vyama vya siasa mkoani Mbeya wameombwa kuwaonya waumini wao kutojihusisha na vitendo vyovyote vya vitakavyosababisha uvunjifu wa awami katika kusherehekea sikukuu ya mwaka mpya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi Diwani Athumani amesema kwa mamlaka waliyo nayo viongozi hao wanayo nguvu ya kuwaonya wafuasi wao kusherehekea sikukuu hiyo kwa amani na utulivu. Alitoa pia wito kwa wananchi wote kuepuka ushawishi wa wa watu wachache wa kujihusisha na vitendo vya uvunjaji wa amani na utulivu akisema jeshi hilo halitosita kuwachukulia hatua za kisheria watakaobainika. “Tunatambua katika kusherehekea sikukuu hiyo wapo baadhi ya watu ambao huitumia vibaya.Jeshi la polisi tumejipanga kukabiliana na watu wote watakaoonesha nia ya kufanya vitendo hivyo” alisema. “Vitendo kama vurugu za kisiasa, mifarakano ya kidini, kujichukulia sheria mkononi, kuchoma matairi kwenye barabara havikubaliki na hatutavumilia.Ni kinyume na utaratibu wa sheria na ni kuisababishia serikali hasara kubwa kwani barabara hizo zimejengwa kwa mamilioni ya kodi za watanzania” Kamanda huyo pia aliwaonya watumiaji wa barabara hususani wanaoendesha vyombo vya moto kuwa makini kwa kufuata sheria za usalama barabarani, kuacha kunywa wakati wanaendesha na kuwa vyanzo vya ajali barabarani na kuwasababishia watu wengine ulemavu ama kupoteza maisha. Kwa upande wao wazazi aliwataka kuwa makini na watoto wao na kuona uwezekano wa kutokwenda nao kwenye kumbi za starehe, kutoacha nyumba zao bila waangalizi, watoto kutembea barabarani bila usimamizi wao. Alisisitiza kila mmoja kuchukua tahadhari katika kipindi hiki kwani wahalifu wanaweza kutumia udhaifu wao kukamilisha azima yao ya kuwavunjia nyumba zao na kuiba ama maeneo yao ya kibiashara kutokana na kukosekana ulinzi. Aliwaomba wananchi wote kutoficha wahalifu bali watumie uzalendo wao kuwafichua wahalifu hao kwa kutoa taarifa katika vituo vya polisi vilivyokaribu na maeneo yao kwa usalama wa mali zao na za wengine na kwamba iwapo kuna uwezekano taarifa hizo za kiuhalifu / wahalifu zitolewe kabla ya kutokea.

No comments:

Post a Comment