Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Saturday, July 25, 2015

MARY MWANJELWA ATETEA KITI CHA UBUNGE VITI MAALUMU MKOA WA MBEYA




ALIYEKUWA Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Mbeya, Dk. Mary Mwanjelwa amefanikiwa kutetea kiti chake baada ya kuwabwaga wapinzani wake 10 kwa kujinyakulia kura 505 kati ya 623 sawa na asilimia 97.

Nafasi ya pili imechukuliwa na Mary Mbwilo aliyejinyakulia Kura 192 akifuatiwa na Hilda Ngoye(164),Priscila Mbwiga(135), Maryprisca Mahundi(120), Shiza Mwakatundu(42), Suma Fyandomo(35), Rhoda Mwamunyange(21),Tusubilege Jengela(19),Joyce Mwang’onda (11) na Neema Kasambala(5).

Kwa mujibu ya matokeo hayo yaliyotangazwa  mbele ya  mgeni rasmi ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Nyerembe Munasa na Katibu wa Chama cha mapinduzi Mkoa wa Mbeya Alhaji Mwangi Kudya jumla ya wajumbe waliopiga kura walikuwa 625 ambapo kura mbili ziliharibika na kura halali 623.

Mbali na kuchagua wabunge wawili wa viti maalumu Mkoa wa Mbeya ambao ni Dk. Mary Mwanjelwa na Mary Mbwilo wajumbe wa Mkutano huo wa UWT pia iliwapitisha wagombea wawili waliopita bila kupingwa  katika nafasi za wabunge wa viti maalum kuwakilisha walemavu na kutoka katika asasi zisizokuwa za kiserikali.

Wabunge hao ni Devotha Mtonyole anayewakilisha Mashirika binafsi kutoka Mkoa wa Mbeya na Lupi Mwaswanya anayewakilisha kundi la wanawake wenye ulemavu ambao hawakuwa na wapinzani katika uchaguzi huo hivyo wajumbe kuwapitisha kwa kauli moja bila kuwapigia kura za ndiyo au hapana.

Kwa upande wake Dk. Mary Mwanjelwa aliwashukuru wapiga kura kwa imani yao kwake ambapo aliwaahidi kutowaangusha katika kipindi cha miaka mitano atakapokuwa Mbunge akiwawakilisha Wanawake wa Mkoa wa Mbeya.

No comments:

Post a Comment