TASINIA ya habari mkoani
Mbeya imepata pigo kufuatia kifo cha mtangazaji Clemence Mpepo(Mzee wa
Makabila) wa kituo cha redio cha Bomba FM cha jijini Mbeya.
Mpepo alifariki usiku wa
kuamkia Novemba 28 mwaka katika hospitali ya taifa ya Muhimbili jijini Dar es
salaam alikokuwa amelazwa akiendelea kupata matibabu kufuatia maradhi ya mapafu
yaliyokuwa yakimsumbua.
Enzi za uhai wake mtangazaji
huyo alijipatia umaarufu mkubwa kwa mashabiki mkoani hapa na maeneo ya jirani
kufuatia umahiri wake wa kutangaza kipindi cha nyimbo za asili ambapo alikuwa
mtaalamu wa lugha za makabila mbalimbali hali iliyokuwa ikiwavutia wasikilizaji
wengi wa kipindi hicho kilichokuwa kikirushwa kila siku ya jumamosi.
Akizungumzia kifo hicho
Meneja wa redio Bomba Fredy Helbert alisema ofisi imepokea kifo hicho kwa
masikitiko makubwa kutokana na ushirikiano mkubwa aliokuwa nao Mpepo mpaka
anaanza kusumbuliwa na maradhi.
Alisema marehemu alianza
kuugua siku chache baada ya kufunga ndoa hivi karibuni akiwa bado katika likizo
ya ndoa na baadaye hali ilizidi kuwa mbaya na kulazwa katika hospitali ya Mkoa
na hatimaye Rufaa Mbeya kabla ya kupelekwa Muhimbili.
“Alikuwa bado katika likizo
ya ndoa hivyo hata kazini alikuwa hajaanza kuingia ndipo maradhi yalipoanza
kumsumbua.Jambo lililokuwa likitupa matumaini kuwa mpaka anaondoka na mkewe
kwenda Dar es salaam alikuwa na unafuu mkubwa.Alikuwa akizungumza vizuri na kucheka
nasi kama tulivyokuwa tumemzoea.Ghafla
tukapata taarifa hali imebadilika na leo tunazungumza msiba”.
“Ni masikitiko makubwa kwetu kama wafanyakazi wenzake.Hakuwa mtu wa kukorofishana na
mtu.Mcheshi wakati wote Lakini kikazi pia japo siku hizi watu wanasema pengo
linazibika kwa Mpembo kwakweli ni vigumu maana utangazaji wake ulikuwa si wa
kipindi kimoja.Kila kipindi tulichompa kilipata wasikilizaji wengi” alisema.
Kwa mujibu wa meneja huyo
Mpepo atazikwa siku ya jumamosi Kinyelezi jijini Dar es salaama kutokana na
maamuzi ya wazazi wake.
No comments:
Post a Comment