Monday, August 19, 2013
KANDORO MGENI RASMI MKUTANO WA JUMUIYA YA AHMADIYYA KESHO MBEYA
MKUU wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro kesho(Agosti 20) anataraji kuwa
mgeni rasmi kwenye mkutano wa jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya wenye
lengo la kuzungumza mchango wa dini katika kuleta amani ya taifa na
dunia kwa ujumla.
Katika kikao chake na waandishi wa habari kiongozi mkuu wa Ahmadiyya
nchini Tahir Mahmood Chaudhry amesema mkutano huo utakaoanza majira
alasiri utafanyika katika ukumbi wa Mkapa jijini Mbeya.
Chaudhry amesema Watendaji kadhaa wa serikali katika ngazi mbalimbali
mkoani hapa pamoja na viongozi wa jumuiya za kidini na asasi zisizo za
kiserikali wamealikwa kwenye mkutano huo na baadhi yao watapata nafasi
ya kuchangia mada hiyo muhimu.
Amesema jumuiya hiyo inauona mkutano wa aina hiyo kuwa muhimu hasa
katika kipindi hiki ambacho taifa linapita katika wakati mgumu wa
mivutano baina ya wanadini wenyewe kwa wenyewe na wakati mwingine na
serikali yao.
Kiongozi huyo pia amelalamikia mapokeo yasiyo sahihi ya tafsiri za
vitabu vitakatifu ikiwemo Kurani kwa baadhi ya wanadini hali aliyosema
ni chanzo cha migogoro mingi inayoendelea duniani.
Ametaja suala la baadhi ya waumini wa madhehebu ya kiislamu kutumia
nguvu na vurugu wakidai ni njia sahihi na kupigania uislamu jambo
alilosema si la kweli na kurani haifundishi hayo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment