Tuesday, August 6, 2013
ZIARA YA KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI ZA MITAA WILAYANI MBARALI
HALMASHAURI ya wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imepata wakati mgumu
mbele ya kamati ya bunge ya hesabu za serikali za mitaa(LAAC) baada ya
kamati hiyo kuutaka uongozi wa halmashauri kueleza sababu ya wao pekee
kupata hati chafu katika mwaka wa fedha uliopita.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Rajab Mohamed Mbarouk aliitaka pia halmashauri
kueleza wamejipanga vipi kuahikisha hawakumbwi na dhahma hiyo kwa mara
nyingine huku akiwakumbusha kuwa walianza kwa kupata hati ya
mashaka,ikafuatia hati safi na mwaka uliofuata waakapata chafu.
Maswali hayo ya mwenyekiti na wajumbe wengine watatu yalisababisha
mkurugenzi Adam Mgoi na mwenyekiti wa halmashauri hiyo Keneth Ndingo
na wataalamu wengi kulazimika kutafuta majibu huku wote wakiwatupia
lawama watumishi watano waliofukuzwa kazi hivi karibuni akiwemo mtunza
hazina kuwa chanzo cha kupata hati hiyo.
“Kwakweli mwenyekiti lazima tuseme ukweli.Mweka hazina aliyekuwepo
alikuwa tatizo kubwa na ndiyo sababu tulipobaini mapungufu yake
tukaamua kumtimua mapema” alisema Ndingo.
Hata hivyo Mwenyekiti wa kamati alionesha kutoridhishwa na majibu hayo
na kumwambia Ndingo kuwa walistuka kukiwa kumekucha na pesa za
wananchi zikiwa zimekwenda na maji.
Hali hiyo ikamlazimu mkurugenzi wa halmashauri Adam Mgoi kuokoa jahazi
kwa kueleza mikakati mbalimbali ambayo imewekwa ili kuinusuru
halmashauri yao na aibu ya kupata hati chafu.
Aliitaja baadhi ya mikakati kuwa ni pamoja na utunzaji sahihi wa
kumbukumbu za mapato na matumizi tofauti na awali ambapo zilihifadhiwa
kienyeji ama kufichwa wakati wakaguzi walipokwenda kufanya kazi yao.
“Kwa sasa tunawahakikishia tunao utaratibu mzuri wa udhibiti wa ndani
wa nyaraka zetu.Tumeboresha pia mfumo wa malipo ya ndani.Ili
kuhakikisha tunafanya kazi zetu kwa ufasaha tumelazimika kuazima
watumishi wawili wa idara ya uhasibu kutoka wilaya jirani ya Chunya
ambao tunasaidiana nao kwa sasa”. Alisema mkurugenzi huyo
Majibu ya mkurugenzi huyo yalionesha kidogo kuwapa moyo wajumbe wa
kamati na mwenyekiti wake kusisitiza kuwa mikakati madhubuti
inahitajika kwakuwa ni aibu kubwa kwa halmashauri hiyo kupata hati
chafu pekee kati ya halmashauri zote nchini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment