Saturday, June 1, 2013
MADIWANI WA CHADEMA WAGOMA MKOA WA MBEYA KUGAWANYWA
kWAKATI mchakato wa kuugawa mkoa wa Mbeya ukiendelea kwa wadau
mbalimbali wakiwemo madiwani kutoa maoni yao kabla ya kufanyika kwa
kikao cha Ushauri cha mkoa(RCC) madiwani wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo(Chadema) katika halmashauri ya jiji wameibuka naa jambo
jipya.
Madiwani hao walionesha utofauti kwenye kikao cha balaza la madiwani
kilichofanyika jana ambapo kila madiwani wa chama kimoja walipaswa
kuwasilisha maoni yao ya namna ya kuugawa mkoa,jina la mkoa
mpya,wilaya zinazopaswa kuzalishwa kutokana na mgawanyo huo pamoja na
makao makuu ya mkoa mpya.
Kikiwa inakaribia kumalizika ndipo katibu wa balaza hilo kaimu
mkurugenzi wa halmashauri ya jiji Dk.Samwel Lazaro alisema maoni
yaliyowasilishwa na madiwani wa Chadema ni kuwa hawaoni sababu ya
kuugawa mkoa wa Mbeya.
Kwa mujibu wa Dk.Lazaro madiwani hao waanaona kuugawa mkoa wa Mbeya ni
mbinu inayotumiwa na viongozi wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi
kugawana madaraka ya kiutawala.
Pia alisema walieleza kufanya hivyo ni kuwapa mzigo mkubwa wananchi wa
kugharamia malipo ya mishahara na matumizi mingine katika ofisi hizo
mpya za mikoa na wilaya.
“Katika maoni yao wao wamesema badala ya rais kuugawa mkoa wa Mbeya na
kuwa mikoa miwili ni vema akatoa fursa hiyo kwa majimbo yaliyo makubwa
yaweze kugawanywa.Wao wanaamini kugawa majimbo ni njia sahihi ya
kuwasaidia wananchi”
Hata hivyo maoni ya madiwani hao yalionekana kupokelewa kwa hisia
tofauti na wajumbe wengine wa kikao hicho hususani madiwani wa CCM na
NCCR Mageuzi ambao walilazimika kuonesha mshangao mkubwa na kuwaona
wenzao kaama miongoni mwa wadau wasioutakia maendeleo mkoa wao.
Akizungumzia maoni hayo meya wa jiji hilo Athanas Kapunga alisema ni
jambo la kushangaza kwa watu wanaotambua fika ukubwa wa mkoa wa Mbeya
unaoongoza kati ya mikoa yote nchini wakanzisha hoja ya kupinga
kuugawanya.
Alisisitiza kuwepo na umuhimu mkubwa wa kuugawa mkoa wa Mbeya akisema
kutasaidia kuboresha huduma za kijamii sambamba na kukuza demokrasia
kwa wananchi.
Aliwasihi wakazi wa jiji la Mbeya na mkoa kwa ujumla kutokubali
kupotoshwa na wanasiasa walio na misimamo isiyolenga kujenga bali
walione wazo la rais kama busara aliyoamua kuitumia kuwarahisishia
kupata maendeleo.
Kwa upande wa madiwani wa NCCR walipendekeza mkoa ugawanywe na
kupatikana mkoa mpya wa Kiwira utakaoundwa na wilaya za
Rungwe,Kyela,Ileje,Busokelo na Mbarali na maakao makuu yawe Tukuyu
wilayani Rungwe na wilaya zinazosalia zibaki mkoa wa Mbeya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment