Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Friday, June 28, 2013

MTOTO APOTEA KATIKA MAZINGIRA TATANISHI,HISIA ZA KUUAWA ZATANDA KWA JAMII

JINAMIZI la kuibwa kwa watoto limezidi kuukabili mkoa wa Mbeya baada ya mtoto Victor Ngisa(4) wa kitongoji cha Barabarani kata ya Lugelele wilayani Mbarali kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Kwa mujibu wa mama mzazi wa mtoto huyo Grace Muhuzi hadi leo ni siku saba zimepita tangu kupotea kwa mwanaye na juhudi za kumtafuta zinaonekana kutokuwa na mafaninikio. Akizungumza na Lyamba Lya Mfipa kwa njia ya simu Grace alisema mwanaye alitoweka katika mazingira ya kutatanisha tangu juni 22 majira ya saa tatu asubuhi alipokuwa akicheza na watoto wenzake. Mama huyo alisema alimwacha mwanaye nyumbani kwa mama yake mdogo kwakuwa yeye alikwenda msitu uliopo jirani kwaajili ya kufuata kuni kwa matumizi ya nyumbani lakini aliporudi hakuweza kukutana tena na mwanaye huyo hadi leo hii. Alisema baada ya kurudi alikutana na mtoto mkubwa kati ya watatu waliokuwa wakicheza na mwanaye na alipomuuliza akasema wenzake walikwenda kuchuma ubuyu katika vichaka vilivyopo jirani na nyumbani kwao lakini alipojaribu kuwafuata huko akakutana na mtoto mwingine na kuambiwa mtoto Victor alilala kabla hajatokea mtu mmoja aliyevaa koti refu jeusi kuwatisha na wao kukimbia. Alisema baada ya watoto hao kukimbia kwa kutishwa na baadaye kubaini walimuacha mwenzao walirejea kwaajili ya kumfuata lakini hawakumkuta tena hivyo wakawa na imani alichukuliwa na mtu huyo wa jinsia ya kiume aliyewatisha. Grace alisema alilazimika kuwafahamisha majirani na jitihada za kumtafuta mtoto huyo zikaanza mara moja na ndipo walipoanza kukutana na taarifa tofauti tofauti kwa kuambiwa na baadhi ya watu kuwa walimuona mtu mmoja akiwa na mtoto mdogo katika maeneo na nyakati tofauti “Kwa siku ya kwanza tulitafuta mpaka usiku bila mafanikio wala taarifa yoyote.Siku ya pili tukiendelea kutafuta tukakutana na watu wakasema walimuona wakiwa wanaelekea machimboni.Siku ya tatu tukakutana na watu wengine wakasema walimuona msukuma mmoja akiwa na mtoto akimnunulia chakula maeneo ya Madibira.Naumia sana kutomuona mwanangu hadi leo” alisema Grace. Mama huyo alisema si tukio la kwanza kutokea wilayani hapo kwani watoto na hata watu wazima wamekuwa wakipotea katika mazingira ya kutatanisha na miili yao kuokotwa baada ya siku kadhaa ikiwa imeharibika vichakani. Kwa upande wake mwenyekiti wa kitongoji cha Barabarani Ramadhan Mkatilwa alisema alipokea taarifa ya kupotea kwa mtoto Victor Juni 22 mwaka huu majira ya saa 12 jioni na kulazimika kupiga mbiu kukusanya wakazi wa eneo hilo na jitihada za kumtafuta zikaanza. Alisema katika siku zote za kumtafuta mtoto huyo wametumia njia mbalimbali ikiwemo wamiliki wqa pikipiki kusafiri umbali mrefu kutoa taarifa kwa vijiji jirani lakini hakuna mafanikio yoyote. Mwenyekiti huyo alikiri kuwa si mara ya pili kwa tukio la kuibwa kwa mtoto kutokea eneo hilo kwani Mei 2012 mtoto mmoja aliibwa lakini kwakuwa mama yake alibaini mapema akapiga yowe na watu walipokusanyika mtu aliyemuiba akamtelekeza porini na kukimbilia kusikojulikana. Kamanda wa polisi mkoani hapa Diwani Athuman awali alisema hana taarifa za kupotea kwa mtoto huyo na kuomba mawasiliano ya wazazi wa mtoto na ndipo alipoamuru mkuu wa kituo cha polisi wilayani Mbarali kufika eneo husika na kupewa taarifa halisi.

No comments:

Post a Comment