Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Saturday, June 1, 2013

MBEYA YAKABILIWA NA LISHE DUNI

WILAYA ya Mbeya ni miongoni mwa wilaya nchini zinazokabiliwa na changamoto ya lishe duni licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa uzalishaji wa mazao ya chakula. Katibu tawala wa wilaya hiyo Edward Mballa aliyasema hayo na kubainisha kuwa hali hiyo inatokana na mpangilio mbovu wa ulaji wa vyakula uliopo katika jamii ya wanaMbeya. Mballa alisema jamii ya watoto wilayani hapa ndiyo inayoathirika zaidi na ukosefu wa lishe bora hali inayowapelekea kukumbwa na maradhi mbalimbali ikiwemo ya utapiamlo. “Tuna tatizo kubwa sana la upangiliaji wa vyakula kwa watoto wetu.Huwezi amini kama ni sisi tuliopo kwenye wilaya na mkoa ambao kila mgeni anayeingia lazima atoke na mzigo wa aina za vyakula kupeleka mkoani kwake.Hatuwapi lishe bora watoto wetu.Tunasubiri mpaka tuje kufundishwa.Ni jambo la aibu kwa jamii kama yetu iliyobarikiwa neema ya vyakula vya aina mbalimbali” Aliwataka watu walio na uelewa kwenye masuala ya lishe kujivika wajibu wa kila mmoja kuangalia namna ya utoaji lishe unaofanyika katika jamii inayomzunguka na kuweza kutoa elimu kwa wale wasio na uelewa. Alisema kwa kufanya hivyo jamii yote itaondokana na tatizo la lishe duni na kuifanya kuwa yenye afya bora na hivyo kumudu shughuli mbalimbali za kiuchumi kwaajili ya maendeleo ya mtu mmoja mmoja,familia na taifa kwa ujumla. Katibu tawala huyo pia aliwataka wasimamizi wa mradi wa Uhai,Ulinzi na Maendeleo ya Mama na Mtoto(CSDP) unaoendeshwa kwenye kata mbili za wilayani hapa kwa ufadhili wa shirika la kuhudumia watoto duniani(UNICEF) kuhakikisha wanasiammia kwa karibu suala la lishe ikiwa sehemu ya malengo ya utekelezaji wa mradi huo. Kwa upande wake mratibu wa mradi wa CSDP wilayani hapa Afisa Mipango Anyambilile Mwandiga alisema ushirikiano wa pamoja baina ya waratibu,viongozi na wananchi ndiyo utakaowezesha kufanikiwa kwa mradi huo unaolenga kuboresha huduma ya Afya ya watoto na mama wajawazitonhuduma ya maji na usafi wa mazingira katika shule za msingi.

No comments:

Post a Comment