Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Sunday, June 30, 2013

MKUTANO WA WADAU WA BONDE LA MAJI LA ZIWA NYASA ULIOFANYIKA MKOANI NJOMBE

UELEWA mdogo wa masuala ya utunzaji mazingira umetajwa kuwa mongoni mwa changamoto kubwa zinazoikabili ofisi ya maji ya Bonde la ziwa Nyasa. Afisa wa maji wa bonde la ziwa Nyasa Witgal Nkondola aliyasema hayo kwenye warsha ya kupitia na kujadili maoni ya wadau mbalimbali wa bonde hilo iliyofanyika mjini Njombe. Nkondola alisema pamoja na jitihada ambazo zmekuwa zikifanywa na ofisi yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali bado kuna wimbi kubwa la wananchi wasio na uelewa katika suala la utunzaji wa mazingira ikiwamo vyanzo vya maji. “Elimu ya utunzaji mazingira kwa wakazi wa maeneo ya bonde letu bado inahitajika.Wengi wao hawatambui umuhimu wa kutunza mazingira hivyo wameendelea na vitendo vinavyohatarisha uwepo wa vyanzo vya maji.Hii kwetu ni changamoto kubwa” alisema Nkondola. Afisa huyo pia alieleza uhaba wa rasilimali fedha kuwa kikwazo kingine katika utekelezaji wa majukumu ya ofisi ya bonde hilo na kuomba serikali na wadau kuangalia uwezekano wa kuongeza bajeti kuisaidia ofisi iweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Changamoto nyingine alisema ni upungufu wa watumishi wa kda ya maafisa maendeleo ya jamii aliosema ni nyenzo muhimu ambayo wamekuwa wakiitumia kuielimisha jamii juu ya masuala ya utunzaji mazingira. Kwa upande wake mkurugenzi msaidizi idara ya rasilimali maji nchini Naomi Lupimo alisema rasilimali ya maji nchini inazidi kupungua kila siku huku mahitaji nayo yakiongezeka hivyo kuibua changamoto ya uwepo wa mkakati madhubuti wa kukabiliana na hali hiyo. Lupimo alitaja sababu za kupungua kwa rasilimali maji kuwa ni pamoja na ongezeko la watu pamoja na shughuli za kijamii ambazo baadhi zimekuwa zikifanyika pasipo kujali athari za kimazingira. Aliwataka wananchi kutambua kuwa rasilimali maji itazidi kuwepo iwapo tu kutakuwa na uangalifu mkubwa katika kuhakikisha vyanzo vya maji vilivyopo vinalindwa na kutunzwa ipasavyo. Akifungua warsha hiyo ya siku mbili yenye washiriki 70,kaimu katibu tawala wa mkoa wa Njombe Mathias Damish aliwataka wadau kutoa maoni yatakayowezesha uwepo wa msukumo chana wa kuliendeleza bonde la maji la Ziwa Nyasa kwa maslahi ya taifa na dunia kwa ujumla. Miongoni mwa wadau waliohudhuria warsha hiyo ni pamoja na wanahabari,wakurugenzi wa halmashauri,maafisa kilimo,maafisa umwagiliaji na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na utunzaji wa mazingira.

No comments:

Post a Comment