Saturday, July 6, 2013
BANKI YA POSTA YATOA MIFUKO 100 YA SARUJI KUNUSURU WANAFUNZI KATIKA SHULE YA MSINGI UHURU TUNDUMA KUKAA KWENYE VUMBI
BENKI ya posta nchini imetoa msaada wa mifuko 100 ya saruji yenye
thamani ya zaidi ya shilingi milioni 7.2 kwaajili ya kukamilisha
ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika shule ya msingi Uhuru
iliyopo Tunduma wilayani Momba.
Mhasibu wa benki ya posta tawi la Mbeya Felix Mapunda,alimwajkilisha
Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo nchini kukabidhi mifuko hiyo jana.
Mapunda alisema suala la kujitolea ni moja ya majukumu ya benki hiyo
kwa ajili ya kuisadia jamii katika nyanja zote hususani nyanja ya
elimu kwa watanzania ikiwa ni njia pia ya kurejesha faida wanayoipata
kwa wananchi.
Hata hivyo alisema benki hiyo imeshawishika kutoa msaada huo kufuatia
kilio cha wakazi wa mtaa wa Uhuru ilipo shule hiyo walichokipeleka kwa
uongozi wa benki wakiomba kuongezewa nguvu ili kukamilisha ujenzi kwa
wakati.
“Wananchi mlifika mkaomba kusaidiwa.Kwakuwa tuliona na ninyi
mmeonyesha moyo wa kujitoa kwa kujenga vyumba vya madarasa
matatu,tukaona tuna kila sababu ya kuwaongezea nguvu.Ndiyo sababu leo
hii tuko hapa na tunawakabidhi kile mlichoomba”.alisema Mapunda.
Aliutaka uongozi unaohusika na ujenzi katika shule hiyo kuitumia
saruji hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa hasa ujenzi wa sakafu kwakuwa
madarasa kwa sasa yanatumika yakiwa na vumbi chini.
Kwa Upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, June Mwandambo, alisema
msaada huo ni sehemu ya mchango mkubwa kwa shule hiyo ambayo
imeanzishwa mwezi april Mwaka huu ikiwa na wanafunzi 175 kuanzia
darasa la kwanza hadi la tatu.
Aidha mwalimu Mwandambo alisema shule hiyo inakabiliwa na changamoto
nyingi ikiwemo majengo yake kutokamilishwa kwa kuweka madirisha hali
inayowafanya wanafunzi pamoja na walimu kupigwa na baridi kali wakati
wote.
Alisema kutokana na uhaba wa dawati ambapo hadi sasa zipo 11pekee
inawalazimu wanafunzi wengi kukalia tofali wanazoweka kwenye sakafu ya
vumbi na kuandikia kwenye magoti.
Naye diwani wa kata hiyo ya Tunduma, Frank Mwakajoka, kwa niaba ya
wananchi wake aliishukuru benki hiyo kwa kutoa mifuko hiyo ya saruji
huku akiihakikishia benki kuwa saruji hiyo itatumika kwa matumizi
yanayo kusudiwa na wala si kwa matumizi mengine.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment