Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Monday, May 21, 2012

WALALAMIKIA BARABARA YA LAMI KUKARABATIWA KWA UDONGO

WADAU na watumiaji wa barabara ya kutoka kituo kikuu cha mabasi kuelekea  eneo la Hospitali ya wazazi  ya Meta wameilalamikia halmashauri ya Jiji la Mbeya mkoani hapa kwa kuendelea kufanya ukarabati wa barabara hiyo ya lami kwa kutumia udongo.

Wadau hao walitoa malalamiko hayo walipo kuwa wakizungumza kwa nyakati tofauti  na waandishi wa habari walikuwa katika mafunzo ya habari za uchunguzi jijini Mbeya yaliyoandaliwa na Umoja wa klabu za waandishi wa habari nchini(UTPC) chini ya uratibu wa Chama cha waandishi wa habari mkoani hapa(MBPC).

Walionesha kushangazwa na hatua ya halmashauri kukarabati barabara  mara kwa mara kwa kutumia udongo hali ambayo imekuwa ikichangia kuwepo kwa  usumbufu kwa watuiaji hao.

Walifafanua kuwa  katika kipindi cha mwenzi Januari hadi Mei barabara hiyo imefanyiwa ukarabati  mara nne kwa kutumia udongo  jambo linalowakera na kuda kuwa ni ufujaji wa fedha za umma.

Mmoja wa watumiaji wa barabara ambaye ni dereva tax Patrick Mbilikile  alisema hali ya barabara hiyo kwa sasa ni mbaya na kuwasababishia gharama za  matengenezo ya mara kwa mara  ya  magari yao.

 “Nashindwa kuielewa serikali yangu japo imenikuza lakini mambo inayoyafanya kutokana na kodi zetu hayalengi kutuletea maendeleo.Sijawahi kuona bara bara ya lami inakarabatiwa kwa kuwekwa udongo sasa halmashauri yetu tangu mwaka jana inafanya ukarabati wa aina hii  na kusababisha bara bara isidumu hali hii inatupa hasara kubwa sisi ambao magari yetu yanaharibika mara kwa mara”alisema Mbilikile.

“Tunauliza kama ushuru wa maegesho tunalipa na kodi  nyingine zote sasa kwanini halmashauri isijipange ikajenga bara bara hii upya badala ya kuendelea kuijaza udongo”aliongeza.

Mmoja wa Madereva wa dala dala zinazotoa huduma za usafiri  Jijini  hapa Castor Mwambembela alisema kuwa kinachofanywa na halmashauri kwa bara bara hiyo ni sawa na utani kwani  licha ya ukarabari wa namna hiyo kufanyika mwaka jana kwa vipindi tofauti na kuonyesha kutokuwa na ufanisi bado inaendelea na ukarabati wa aina hiyo.

Aliongeza kuwa katika ukarabati wa mwaka jana  kuna wakati walijaribu kutumia Zege iliyochanganywa na Saruji katika kuziba vilaka lakini bado haikuweza kudumu hivyo fedha za walipa kodi kuendelea kupotea pasipo mabadiliko yeyote.

Kwa upande wake abiria wa daladala Christina Ikusya alisema bara bara  zilizopo jijini  Mbeya  hazivutii hivyo ni changamoto kwa halmashauri kujipanga na kuhakikisha inazijenga katika kiwango kinachoendana na hadhi ya Jiji.

Aidha waandishi wa habari walishuhudia ukarabati  ukiendelea kwa kutumia udongo ambapo mafundi waliokuwa wakiendelea na kazi hiyo walipohojiwa kuhusu ukarabati, walisema wanafanya hivyo ili kuziba mashimo  kuondoa usumbufu kwa watumiaji wa barabara wakati  matengenezo makubvwa yakisubiriwa.
Mmoja wa wafanyakazi hao ambaye alikataa kutaja jina lake kwa madai kuwa yeye si msemaji alibainisha kuwa barabara hiyo inatarajiwa kufanyiwa ukarabati mkubwa kwa kiwango cha lami hivi karibuni, ingawa hakutaja ni lini.

Hata hivyo juhudi za kumpata Mkurugenzi wa jiji kuzungumzia suala hilo hazikuzaa matunda`baada ya kumkosa ofisini kwake na alipotafutwa kwa njia ya simu yake ya kiganjani  alijubu kwa ujumbe mfupi kuwa yupo kwenye kikao na kuwa atapiga simu mara baada ya kikao.
Mwisho

No comments:

Post a Comment