Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Wednesday, January 22, 2014

RC KANDORO AKABIDHI MSAADA WA NAFAKA KWA KITUO CHA KULELEA YATIMA

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbass Kandoro akikabidhi msaada wa mahindi na maharagwe kwa mkuu wa kituo cha kulelea watoto Yatima cha Malezi ya Huruma kilichopo Simike jijini Mbeya Anna Kasile.Kituo hiki kinalea jumla ya watoto Yatima 120 ambapo wapo waishio kituoni hapo na pia wanaosoma katika shule mbalimbali za sekondari nchini Mkuu wa mkoa akimpongeza mama huyu kwa kuendelea kutoa mchango wake kwa jamii inayomzunguka kwa kuwalea yatima.Kandoro aliitaka jamii nyingine kushiriki katika kuwalea watoto hao akisema ni jamii isiyopaswa kutengwa. Mkuu wa mkoa akiwa amemshika mtoto Judith ambaye ni mmoja kati ya watoto wawili wachanga wanaolelewa kituoni hapo wakiwa walipelekwa kutoka maeneo tofauti MKUU wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro ametoa msaada wa vyakula kwa kituo cha kulelea watoto yatima cha Malezi ya Huruma kilichopo maeneo ya Simike jijini hapa. Vyakula alivyokabidhi mkuu huyo wa mkoa ni mahindi gunia mbili,mchele gunia moja na maharage gunia moja. Akikabidhi msaada huo,Kandoro aliitaka jamii kushiriki katika malezi ya watoto yatima kwakuwa watoto hao wana mahitaji kama ilivyo kwa watoto walio na wazazi wote. Alisema jamii inapaswa kushiriki kikamilifu kuwalea watoto yatima kwa kuzingatia kuwa na wao hawakupenda kuishi pasipo uwepo wa wazazi wao ambao wangeweza kuwapa malezi bora kama wangekuwa hai. “Malezi ya watoto yatima si jukumu la mtu mmoja.Kila mwana jamii anapaswa kulitambua hilo na kutoa mchango wake kuwatunza kama anavyofanya kwa watoto wetu majumbani.Watoto hawa nisehemu ya taifa letu,hatupaswi kuwabagua na kuwaacha wakipata shida” alisema Kandoro. Aliahidi kuendelea kuihimiza jamii ya wakazi mkoani hapa kuendelea kuchangia vituo vinavyolea watoto yatima ili kuwasaidia wale waliojitoa kuwalea katika vituo vyao. Alimpongeza mkuu wa kituo hicho Anna Kasile kwa kuchukua maamuzi ya kuungana na familia ya watoto yatima kwaajili ya kuwalea mara tu alipostaafu katika ajira yake serikalini. Akipokea msaada huo,Kasile alisema zipo changamoto nyingi katika kuwalea watoto yatima na kuomba serikali na jamii kwa ujumla kutoa ushirikiano wa thati ili kufanikisha malezi hayo. Alisema kituo hicho hivi sasa kinalea watoto 120 wakiwemo waliopo kituoni hapo na wale wanaosoma katika shule mbalimbali nchini zikiwemo za sekondari.

No comments:

Post a Comment