Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Saturday, March 17, 2012

KILUFI,MWANJALE,NGOYE WAMKOROMEA WAZIRI MAIGE


 WAZIRI wa Maliasili na Utalii Ezekiel Maige leo amepata wakati mgumu kujibu malalamiko yaliyotolewa na wadau waliohudhuria kikao cha kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya kimipaka ya hifadhi ya taifa kilichofanyika jijini Mbeya baada ya kuelezewa vitendo viovu wanavyofanyiwa wananchi na maafisa kutoka idara za wizara yake.

Wabunge mchungaji Luckson Mwanjale (Mbeya vijijini),Dickson Kilufi(Mbarali) na Hilda Ngoye(Viti maalum CCM) aliyemwakilisha mbunge wa jimbo la Rungwe Mashariki Mark Mwandosya ni miongoni mwa wadau walioibua hoja nzito katika kikao hicho kilicjhofanyika katika ofisi za mkuu wa mkoa.

Mchungaji Mwanjale alisema ushirikiano hafifu kati ya maafisa wa hifadhi ya taifa ya Kitulo na vijiji jirani umesababisha mgogoro wa kimpaka kati ya hifadhi hiyo na wakazi katika kijiji cha Kikondo kuwa mkubwa kiasi cha kuitia doa serikali ya wilaya pamoja nay eye mwenyewe.

Mbunge huyo alisema hali ni mbaya katika kijiji hicho ambapo yeye mwenyewe ama mkuu wa wilaya kufika kijijini hapo kwa sasa ni ngumu kutokana na kuonekana na wakazi hao kama watu wasiowatetea kutokana na mgogoro unaoendelea.

Hsata hivyo alisema hasira zaidi ya wananchi hao inatokana na vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na maofisa waliopo katika hifadhi hiyo hasa vya kukamata mifugo ya wakazi na kuwatoza faini kubwa tofauti na sheria zinavyoeleza.

“Lakini pia tunazidi kupata wakati mgumu sisi wawakilishi wa wananchi maana mgogoro huu umekuwa wa muda mrefu na leo hii mimi na wenzangu madiwani tulikuwa tumewaahidi kuwa waziri utafika na kuzungumza nao ili walau na sisi tupumue.Sasa unaposema tena huwezi kwenda sisi sijui hata tunarudi na jibu gani la kuwaridhisha” alisema

Akizungumzia chanzo cha mgogoro huo,alisema kinatokana na kutowepo kwa mpaka maalumu unaotenganisha hifadhi na eneo la wananchi,Tanapa kuendelea kudai kuwa ilikwisha lipa fidia na kuwataka wakazi wahame huku wananchi walioishi katika kijiji hicho kwa zaidi ya miaka 30 wakisema hawajalipwa chochote.

Naye mbunge Ngoye alisema mgogoro kati ya hifadhi ya Kitulo na wananchi wa vijiji vya wilaya ya Rungwe umekuwa wa muda mrefu na unatokana na vitendo vya kinyanyasaji vinavyofanywa na maofisa wa hifadhi,kutofautiana kwa taarifa za mpaka.

Kwa upande wake mbunge wa Kilufi alilalamikia migogoro ya mipaka kati ya hifadhi kutomalizwa haraka kwa serikali kuhakikisha inaivalia njuga na kuimaliza kabisa ili kuwapa nafasi wananchi kuendelea na shughuli za kimaendeleo.

Naye mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbarali alilalamikia sheria ya fidia akisema imepitwa na wakati kiasi kwamba wananchi wanaoondolewa kwenye maeneo yao wanalipwa fedha kidogo zisizowawezesha kununua ardhi mahala pengine na kujenga makazi.

Waziri Maige alisema kuahirisha kwake kwenda Kikondo kunatokana na tume aliyoiunda awali kwenda kufanya tathmini ya mgogoro uliopo kutowashirikisha wadai ilipofika kijijini hapo hali inayolazimu kazi hiyo kufanywa upya wazo lililoungwa na mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro.

No comments:

Post a Comment