Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Wednesday, March 21, 2012

WAKAZI wa baadhi ya mitaa ya kata ya Isanga jijini Mbeya wamekosa huduma ya maji safi na salama kwa kipindi cha takribani mwezi mmoja sasa.

Hali hiyo inatokana na mabomba ya maji yaliyo chini ya mamlaka ya maji safi na taka jijini Mbeya Mbeyawssa kutotoa maji katika kipindi hicho chote huku wakazi hao wakiwa hawana taarifa ya nini chanzo cha kukosa huduma hiyo.

Wakizungumzia hali hiyo wakazi hao wameilalamikia mamlaka husika kwa kushindwa kuwapa taarifa juu ya nini chanzo cha kuwakatia huduma hiyo na kuwaacha wakiishi maisha ya sintofahamu.
 
Mmoja wa wakazi hao aliyejitambulisha kwa jina la mama Neema amesema hivi sasa wanalazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya maji tena katika visima vilivyo na maji wanayoamini kuwa si salama kwa matumizi ya majumbani.

“Tulizoea kupata maji safi na salama lakini tumekatiwa huduma hiyo na hatujui tatizo ni nini.Tunalazimika kwenda kufuata maji katika visima vya kuchimwa kwa mkono vilivyopo katika bonde la Ilolo ambako mvua inaponyesha takataka zote za kutoka kwenye makazi ya watu ndiko zinapelekwa na maji ya mvua” anasema

Mkazi mwingine Priscar Robert amesema tangu huduma hiyo ikatwe hakuna ofisa yeyote wa mamlaka husika aliyefika na kueleza tatizo ni nini na litadumu kwa muda gani ili waweze kujipanga.

Akizungumzia malalamikoa hayo kwa njia ya simu,ofisa habari wa Mbeyawsa Mary Sayula awali amesema hawajui kama kuna tatizo hilo lakini baada ya kuzungumza na maafisa wenzake akasema hali hiyo inatokana na kuharibiwa kwa miundombinu ya maji kulikosababishwa na uboreshaji wa barabara ya katikati ya eneo la Isanga unaoendelea.

Mtandao huu umefika katika eneo hilo na kukuta miundombinu mingi ya maji iliyoharibiwa huku barabara iliyotajwa na ofisa huyo ikiendelea kukarabatiwa.

No comments:

Post a Comment